MOFOLOJIA YA KISWAHILI SANIFU

Katika somo hili tutajifunza kwa kina mada ya Mofolojia ya Kiswahili ya Kiswahili sanifu kwa kungalia vipengele vifuatavyo: mawanda ya mofolojia, fasili za dhana mbalimbali za msingi za kimofolojia kama mofolojia, mofu, alomofu na mofimu, uhusiano wa mofu na mofimu, kubainisha mofu katika lugha ya Kiswahili na kufafanua njia za uundaji wa maneno.

Fasili ya dhana za Msingi za Kimofolojia

Dhana ya Mofolojia Wanaisimu wengi wamewahi kuishughilikia dhana ya mofolojia kwa kina. Zifuatazo ni fasili mbalimbali kwa mujibu wa wanaisimu hao:

Mathew (1974) anasema kwamba mofolojia ni tawi la taaluma ya isimu ambalo huchunguza maumbo ya maneno hususani maumbo ya mofimu.

Hertman (1972) naye anasema kuwa mofolojia ni tawi la sarufi hushughulika na uchunguzi na uchambuzi wa maumbo, fani na aina za maneno yalivyo sasa pamoja na historia zao.

Richard na wenzake (1985) wanasema kuwa mofolojia inaweza kupewa maaana kuu mbili yaani:

(i) Mofolojia huchunguza mofimu na alomofu zake na jinsi ambavyo hukaa pamoja na kuunda maneno mbalimbali katika lugha zinamotumika.

(ii) Mofolojia ni mfumo kamili wa mofimu katika lugha fulani. Kwa namna hii tunaweza kuzungumza juu ya mofolojia ya lugha Kiingereza au mofolojia ya Kijerumani

TUKI (1990) wanafasili mofolojia kama tawi la isimu ambalo huchunguza maneno na aina zake.

Tunapozichunguza kwa makini fasili zilizotolewa hapo juu tunaona ya kuwa mofolojia inapewa sura kubwa mbili yaani:

Mofolojia kama taaluma ya isimu/ sarufi ambayo inalo jukumu la kuyachunguza maneno ili kuyaelewa yake yalivyo

Mofolojia kama kiwango kimojawapo cha kila lugha. Kiwango cha mofolojia kinatofautiana na viwango vingine vya lugha ambavyo ni fonolojia, sintaksia na semantiki. Wakati mwingine wataalamu wengine hukiweka kiwango hiki pamoja na kile cha sintaksia.

Dhana za mofu, alomofu na mofimu ndizo ambazo hutumiwa sana kwa uchambuzi wa kiisimu hususani katika kiwango cha mofolojia. Isilahi hizi zote tatu zimetoholewa kutoka istilahi za Kiiingereza yaani Mofu- kutoka neno la Kiingereza morph, alomofu kutoka neno la Kiingereza allomorph na mofimu kutoka neno la Kiingereza morpheme. Yafaa dhana hizi tatu zielezwe vizuri kwa sababu ni dhana muhimu sana katika isimu.

1.1.1 Mofimu

Dhana ya mofimu imejadiliwa na wataalam mbalimbali. Crystal (1971) anasema kuwa mofimu ni kipashio kidogo kabisa katika uchambuzi, mara walibuni na kuanza kuitumia dhana ya mofu. Badala ya uchambuzi kuishia kwenye neno tu, uchambuzi ukawa unaendelea hadi kwenye kiwango cha mofimu.Crystal 1971, Kayuza 1988, Marealle 1978 na Mohamed (1986) wanafuata mtazamo huu wa dhana kabla ya Sarufi Zalishi kama inavyoonyeshwa kwenye maelezo yafuatayo: Marealle (1978) anafasili neno mofimu kama kipashio kidogo kabisa cha kisarufi kilicho na Mohamed anafasili mofimu kama kijineno au sehemu ndogo ya tamko iletayo maana kamili. Kayuza (1988) anasema kuwa mofimu ndiyo ngazi ya mwisho ya maumbo na pia ni tamko dogo lenye maana kisarufi.

1.1.2 Dhana ya Mofimu baada ya Kuasisiwa kwa Sarufi
Zalishi

Baada ya kuasisiwa kwa sarufi Zalishi katika karne ya 20, dhana muhimu mbili ziliingizwa katika uchambuzi wa mofolojia ya lugha. Dhana hizo ni mofu na alomofu. Baada ya kuingizwa kwa dhana mpya za mofu na alomofu, mofu ilichukuwa maana iliyokuwa imepewa mofimu, kama kipashio kidogo cha lugha kinachobeba au kusetiri maana. Sasa mofimu ikapewa maana mpya. Fasili mojawapo inayotoa hii maana mpya ya mofimu ni ile ya Hartman (1972) ambaye anasema: Mofimu ni kipashio dhahania cha umbo fulani ambacho kinaweza kuwakilishwa kwa mofu tofautitofauti katika mazingira anuwai. Mofimu ya wingi katika Kiingereza, kwa mfano huwa kilishwa kwa mofu /s, /z/, /iz/.

Mofimu kama kitu dhahania
Mofimu ni kipashio dhahania cha lugha na sio umbo halisi kwa sababu hakionekani wala hakiwakilishi kupitia maandishi bali kimo akilini mwa msomaji. Mofimu si umbo la maneno bali ni maana tunazozisetiri akilini mwetu. Kwa maneno mengine, mofimu ni kipashio kidogo kabisa cha kisarufi kilicho na maana.

1.1.3 Mofu
Ni istilahi ambayo imetoholewa kutoka istilahi morph kutoka lugha ya Kiingereza. Nida (1949) anaeleza kuwa, mofu ni umbo la neno ambalo huwakilisha mofimu na ambalo hudhihirika kiothografia. Mofimu ambazo ni elememtni dhahania huwakilishwa na mofu ambazo hudhihirika ama kifonolojia zikiwa ni sauti za kutamkwa au kiothografia zikiwa ni alama za kuandikwa.

Platt (1985) anafasili mofu kama kipashio kidogo kabisa chenye maana katika lugha. Mofu haiwezi kugawanywa katika sehemu ndogondogo zaidi bila kuharibu maana yake. Mofu huwakilisha maana ya kileksika na zile za kisarufi. TUKI (1990) wanasema kuwa mofu ni kipashio cha kimofolojia kiwakilishacho mofimu.

Baada ya kuona fasili zote tatu zilizotolewa na wataalamu
mbalimbali kuhusiana na dhana ya mofu, yapo mabo ya msingi kabisa kuhusu sifa muhimu za kuzingatia zinazopambanua dhana ya mofu. Mambo haya ya msingi yanaweza kuzingatiwa:

(i)Mofu ni sehemu halisi ambazo huwa tunazitamka na kuzinadika wakati tunapoandika maneno lakini maana ambazo huwakilishwa na mofu ndizo tunazoziita mofimu ambazo ndizo huwa dhahania kwa sababu maana hizo huwa hazitamkwa wala kuandikwa.

(ii)Kwa kweli mofu imo katika upande wa utendaji lakini mofimu ni dhana ya kidhahania iliyomo akilini mwa watu na ambayo ni sehemu ya umilisi wa lugha wa kila mtu. Mofimu ni tafsiri ambayo mtu hufanya akilini mwake kuhusu maana ambayo husetiriwa kwenye mofu.

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, mofimu ni kipashio kidogo sana cha neno ambacho kina maana na pia kinaweza kubadili maana ya neno. Hebu tuone mfano wa mofu kama ifuatavyo:


{imb}hubakia {imb} tu mahali popote inapotokea kama:
(i)imb+ a imba
(ii)si+imb+i siimbi
(iii)u+si+imb+e usiimbe
(iv)tu+ta+imb+a tutaimba
Mzizi (toto) pia una mofu moja tu ambayo haibadiliki, kwa mfano,

(i)m+toto (ii) wa+toto (iii) u+toto (iv) u+toto+ni

Mzizi

Mzizi ni mofu ambayo ni muhimu zaidi katika neno na huweza kukaa peke yake kama neno kamili. Aidha, hii ni sehemu ya neno ambayo haibadilikibadiliki. Katika uchanganuzi wa neno, mzizi hauwezi kuchanganuliwa katika sehemu nyingine ndogo bila kupoteza uamilifu na maana yake. Hivyo basi, mzizi ni kiini cha neno na ni sehemu ya neno ambayo maneno mengine huundwa kutoka kwao.

Mzizi wa Kitenzi
Mzizi wa kitenzi ni sehemu ya kitenzi ambayo haibadilikibadiliki wakati wa mnyambuliko. Kiini ni ile sehemu kuu ya kitenzi bila kiambishi chochote. Hii ndiyo sehemu ambayo hubeba maana halisi ya kitenzi. Kwa mfano:
Kitenzi Mzizi
Alipikika {-pik-}
Ulipika {-pik-}
Utapika {-pik-}
Mlipika {-pik-}
Kilipikwa {-pik}

Sifa za Mzizi
(i)Mzizi hufanya neno kuwa na uafifishaji mkamilifu, hivi kwamba mzizi ukiondolewa katika neno, utakopotea.
(ii) Mzizi huweza kukaa yake kama neno kamili, kwa mfano: baba,mbuzi n.k (mofu huru tu).
(iii)Katika lugha ya Kiswahili kuna baadhi ya maneno ambayo huundwa na mwambatano wa mizizi miwili.

Maumbo ya Mizizi katika Lugha ya Kiswahili

(i)Mzizi unaundwa na fonimu moja
Kwa mfano: katika maneno yafuatayo:
Kufa – / f /
Kula / l /

(ii)Mzizi unaounda na fonimu mbili silabi
Mfano katika maneno
Mtu – (-tu-)
Mtoto m- (-to)

(iii)Mzizi unaoundwa na mofimu zaidi ya mbili
Kwa mfano: Cheza (–chez-)
Piga – (-pig-)
Imba (-imb-)
Tembea- (-temb-)

Aina ya Mizizi

Kuna aina kuu mbili za mizizi. Uanishaji huu umekitwa kwenye maana na umbo la mizizi husika.

(a) Mzizi Huru
Mzizi huru ni mzizi ambao huweza kusimama peke yake kama neno lenye uarifishaji mkamilifu ambao hauhutaji kaumbikwa viambishi. Katika lugha ya Kiswahili, kwa mfano, mizizi ya maneno mengi huwa ni mofu huru ambazo zina uwezo wa kukaa peke yao, kama maneno kamili kwa mfano, maneno yafuatayo:


Nomino{baba} 2. {taifa} 3. {Sungura} 4. {shati} 5. {Ndege} 6.
{kaka} 7. {Juma} 8. {Arusha} 9. {Mombasa} 10. {Tanga}

Vivumishi

  1. Rahisi 2. chafu 3. Bora 4. {Imara} 5.{goigoi} 6.
    {mwerevu}

Viwakilishi

  1. {vile} 2. {mimi} 3. {wale} 4. {ninyi] 5. {yeye} 6. {wao}

Vielezi

  1. {upesi} 2.{ haraka} 3. {sana} 4. {leo} 5. {jana} 6. {juzi}

Vihusishi

  1. {pembeni} 2. {ndani} 3. {juu} 4. {nyuma} 5. {chini} 7.
    {kwa} 8. {mbele}


(b) Mzizi Tegemezi


Mzizi tegemezi hauwezi kusimama peke yake bila kiambishi cha awali au tamati na kuleta maana kamili. Kwa mfano :
(-l-) – katika neno kula
(-f-) katika neno kufa
(-j-) katika neno kuja
(-tu-) katika neno mtu
(-pig-) katika nenno piga

Shina

Shina ni mzizi ambao umeambikwa kiambishi tamati. Aidha ni sehemu ya neno inayotumiwa kuunda neno jipya. Shina kamili haliwezi kuchanganuliwa bila kupoteza maana. Kuna aina zifauatazo za shina:

(a) Shina Sahili

Shina sahili ni shina ambalo huundwa na mofu au mizizi huru. Kwa
mfano:
Shamba –mashamba
Taifa – mataifa
Shati – mashati
Jembe -majembe

(b) Shina Changamano

Shina changamano ni shina ambalo huundwa na mzizi mmoja na viambishi, hususani viambishi tamati. Kwa mfano:
Pika – pikia, pikiwa
Piga – piga, pigia, pigana
Cheza – chezea, chezewa, chezeana

(c) Shina ambatano

Ni shina ambalo huundwa kwa muambatano wa mizizi huru miwili. Kwa mfano:

Askari + kanzu ——————askarikanzu
Mwana+ hewa ——————-mwanahewa
Bata + mzinga —————— batamzinga

1.2 Kubainisha uhusiano wa mofu na
mofimu===============================

Mofu ni sehemu halisi ambazo huwa tunazitamka na kuzinadika wakati tunapoandika maneno lakini maana ambazo huwakilishwa na mofu ndizo tunazoziita mofimu ambazo ndizo huwa dhahania kwa sababu maana hizo huwa hazitamkwa wala kuandikwa.

Kwa kweli mofu imo katika upande wa utendaji lakini mofimu ni dhana ya kidhahania iliyomo akilini mwa watu na ambayo ni sehemu ya umilisi wa lugha wa kila mtu. Mofimu ni tafsiri ambayo mtu hufanya akilini mwake kuhusu maana ambayo husetiriwa kwenye mofu. Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, mofimu ni kipashio kidogo sana cha neno ambacho kina maana na pia kinaweza kubadili maana ya neno.

1.3 Kubainisha aina za Mofu katika Kiswahili Sanifu

Ndugu mwanafunzi, kabla hatujabainisha aina za mofu katika
lugha ya Kiswahili, hebu sasa tuchunguze sifa mbalimbali za mofu
kama ifuatavyo:

Sifa Mbalimbali za Mofu

Zipo sifa mbalimbali za mofu katika lugha ya Kiswahili.
Sifa hizo ni

(i)Mofu kama sehemu halisi ya neno

Hii ina maana kwamba mofu ni maumbo halisi ya maneno ambayo hutamkwa wakati watu wanapozungumza au kuandikwa wakati watu wanapoandika maneno. Kwa mantiki hiyo basi, mofu ni umboa halisi ambalo tunaweza kulisikia linapotamkwa na kuliona linappokuwa limeandikwa.

(ii) Mofu hudhihirika kifonolojia na kiothografia

Kwa kuwa mofu ni umbo halisi la neno, basi mofu mbalimbali
hudhihirika kifonolojia zinapotamkwa na pia kimaandishi
zinapoandikwa yaani kiothografia.

(iii)Mofu huwakilisha maana

Hapa tunasisitiza kuwa mofu huwakilisha maana fulani katika neno lolote katika lugha katika lugha yoyote patakuwepo maana na maana hizo huwa zimesetiriwa katika mofu zilizopo katika neno. Hii ina maana kwamba kama kila neno huwa na maana fulani, basi maana hiyo itakuwa imewakilishwa na mofu fulani. Hii ina maana kuwa hakuna neno lolote katika lugha yoyote ambalo linaweza kuwa ni neno lenye maana bila kuwa na mofu angalau moja. Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa kila neno lenye maana katika lugha, litakuwa na mofu angalau moja.

(iv) Mofu ni kipashio kidogo kabisa cha neno chenye maana

Hapa kinachotiliwa mkazo ni ule ukweli kuwa, mofu ni sehemu ndogo kabisa ambayo hubeba maana na kuwa sehemu hiyo haiwezi kugawanywa katika sehemu ndogo zaidi zilizo na maana kuliko. Hapa tungeweza kusema kuwa kwa ukubwa mofu ni umbo ambalo hudhaniwa kuwa ni kubwa kuliko fonimu na ni ndogo kuliko neno.

Aina za Mofu

Aina za mofu zinaweza huanishwa kwa kutumia vingezo vya
maana na mofolojia katika Kiswahili Sanifu. Kwa kutumia kigezo cha maana zipo mofu za aina tatu ambazo ni:

(a) Mofu Huru ( free mofu)
(b) Mofu funge (bound morphs)
(c) Mofu tata (ambiguous morphs

(a) Mofu huru

Weber (1985) anasema ya kuwa mofu huru ni zile mofu ambazo zinaweza kukaa peke yake kama maneno kamili. Mofu huru ni mofu zilizo na uwezo wa kukaa peke yake na zikawa maneno kamili yenye maana.. Mara nyingi mizizi ya baadhi ya maneno ndiyo ambayo ina uwezo wa kukaa peke yake na yakawa maneno kamili yanayojitosheleza. Mizizi ya aina hiyo si lazima iwekwe viambishi ndipo iwe maneno. Katika lugha ya Kiswahili, kwa mfano, mizizi ya maneno mengi huwa ni mofu huru ambazo zina uwezo wa kukaa peke yao, kama maneno kamili kwa mfano, maneno yafuatayo:

Nomino

  1. {baba} 2. {Kuku} 3. {Sungura} 4. {Kalamu} 5. {Ndege} 6.
    {Dada} 7. {Juma} 8. {Kilimnajaro} 9. {Nairobi} 10.
    {morogoro

Vivumishi

  1. Ghali 2. Safi 3. Dhaifu 4. {Imara} 5.{goigoi} 6. {hodari}

Viwakilishi

  1. {mimi} 2. {sisi} 3. {wewe} 4. {ninyi] 5. {yeye} 6. {wao}

Vielezi

  1. {upesi} 2.{ haraka} 3. {sana} 4. {leo} 5. {jana} 6. {juzi}

Vihusishi

  1. {nje} 2. {ndani} 3. {juu} 4. {nyuma} 5. {chini} 6. {ya} 7.
    {kwa} 8. {mbele}

Viunganishi

  1. na, 2. {halafu} 3.{bila} 4. {ila} 5. {aidha} 6.{pia}

Tanbihi

Vitezni vyenye asili ya Kibantu, wakati wote huwa ni tegemezi kwa sababu huhitaji angalau kiambishi tamati kimoja ndipo viwe neno kamili. Namba kwenye mabano inaonyesha idadi ya mofu katika neno. Kwa mfano,

  1. {ruk}+ {a} ruka (2)
  2. 2. {chez} + {a} cheza (2)
  3. {andik} + {a} andika (2)
  4. {imb} + {a} imba (2)

(b) Mofu Funge

Richards et al. (1985) wanaeleza kuwa, mofu funge ni kipashio cha kiisimu ambacho huwa hakikai peke yake bali ni lazima kiandamane na mofu nyingine. Hartman (1972) anasema kwamba, mofu funge ni mofu ambayo haiwezi kutumiwa peke yake kama neno kamili lililo na maana yake bainifu, bali daima hutumiwa kama kiambishi tu kinachoambatana na mzizi au viambishi vingine ili kukamilisha neno. Maana ya mofu funge hutegemea muktadha wa mofu. Kwa hiyo sifa kubwa ya mofu funge ni kuwa mofu funge haiwezi kukaa peke yake ikawa neno kamili. Sifa hii inatofautisha mofu funge na mofu huru kuwa mofu huru ina uwezo wa kukaa peke yake. Mofu funge lazima ziwekwe pamoja na mofu nyingine moja ili kuleta maana kamili ya neno. Hii huwafanya wanaisimu wengine kuziita mofu hizi tegemezi. Mara nyingi hizi mofu funge huwakilisha maana za kisarufi. Kwa mfano katika nomino huweza kuwakilisha maana zifuatazo:

  1. Idadi ya Umoja

(i) M+ toto (m)
(ii) Ki+tabu (ki)
(iii)ji+ cho (ji)

2.Ukubwa wa Nomino

Ji+tu (ji)
Ji +su (ji)

3.Idadi ya Wingi

Wa +toto (wa)
Vi + tabu (vi)
Ma + cho (Ma)

4.Udogo wa Nomino

Ki+ji+tu (ki)
Ki+ji+su (ki)
Ki+ji+ti (ki)

Katika mifano hiyo hapo juu tuanaona kuwa mofu ya ukubwa katika lugha ya Kiswahili huwa ni {ji} ambayo huwekwa pamoja na mzizi wa nomino. Lakini wakati wa kukifanya kitu mkiwe kidogo, mofu mbili hutumika kwa pamoja yaani mofi {ki} ya udogo pamoja na mofu {ji} ya ukubwa, ambapo zikiandamana na mzizi wa nomino ndipo tunapata ile hali ya udogo.

5.Unominshaji wa aina zingine za maneno:

Lima (i) Ku+lim+ a (1) {ku} (2) {a}
(ii)U+ku+lim+a (1) {u} (2) {ku} (3) {a}
(iii)Wa+ku+lim+a

(c) Mofu Tata

Weber (1985) anaeleza mofu tata kama kipashio cha kiisimu
ambacho kinaweza kupewa maana ya moja, yaani maana kauanzia mbili na kuendelea. Vipashio vya kiisimu ambavyo huweza kuwa tata ni mofu, maneno, virai na sentensi. Kwa kuzingatia fasili ya Weber, mofu tata ni mofu ambazo huwa na maana zaidi ya moja, tuseme labda maana kuanzia mbili na kuendelea. Hapa inafaa tutoe mfano wa mofu tata katika lugha ya Kiswahili. Tazama sentensi ifuatayo:

Pendo alimpiga Noel mpira

Sentensi hii ni tata kwa sababu, ina maana au tafsiri zaidi ya moja. Utata wa sentensi hiii si wa kisarufi bali upo katika kitenzi. Kitenzi hiki kina mofu sita.

Aina za mofu kwa kuzingatia Uanishaji kwa kigezo cha
Kimofolojia

Zipo aina mbili za mofu, ambazo ni: (i) Mofu changamani
(ii) Mofu kapa

Mofu changamani

ni mofu inayoundwa kutokana maumbatana wa
mizizi huru miwili au (mashina mawili). Mashina hayo huwa na
usafairishaji mkamilifu. Kwa hiyo, kila shina huweza kusimama
kama neno kamili lenye kujitosheleza kimuundo na kimaana. Kwa
mfano:
(a) Mwana + jeshi ———————-mwanajeshi
{mw-} – ngeli ya kwanza; idadi ya umoja
{-ana-}- mzizi
{jeshi} – mzizi huru
(b) Mwana +idara –mwanaidara
{-mw-} –idadi (umoja)
{-ana-} – mzizi
{idara}- mzizi huru

Mofu Kapa

Mofu kapa haiwakilishwi na kitu au alama yoyote dhahiri. Kwa mujibu wa Massamba (2004) anasema kuwa katika lugha ya Kibantu, viambishi vya ngeli vya nomino zilizomo katika ngeli huwa haviko dhahiri katika neno na katika umoja au wingi. Mofu hizi hazina umbo na hazionekani, haziandikwi wala kutamkwa ila ni sehemu ya umilisi wa watumiaji wa lugha husika. Ijapokuwa mofu hizi hazionekani wala kutamkwa, huwa na maana katika neno
husika. Kwa mfano:

Umoja Wingi
Ukucha kucha
Ukiangalia katika mfano wa hapo juu katika wingi, kiambishi cha wingi hakijitokezi bayana ilhali kiambishi cha cha umoja (-u-) ni bayana.

Dhana ya Alomofu

Richards na wenzake (1985) wanafasiri alomofu kama umbo
mojawapo kati ya maumbo kadhaa tofauti yanayoiwakilisha
mofimu moja. Hartman (1970) anafasiri alomofu kama umbo
badala ya mofimu fulani ambalo halibadili maana. Bauer (1983) ni mofu mojawapo katika seti ya mofu zinazoiwakilisha mofimu fulani ambayo ina mazingira yake ya kifonetiki, kileksika au kisintaksia (kisarufi).

Tukiangalia fasili hizo hapo juu, tunaona kuwa zinaeleza sifa
muhimu zinazofafanua alomofu. Zifa hizo ni kama ifuatavyo:

(i)Alomofu ni umbo halisi ambalo ni sehemu ya neno fulani na mbalo hutamkwa kwa kuandikwa. Kwa hiyo alomofu ni mofu na sifa tulizozitoa kuhusu mofu ndizo ndizo zinazofaa pia keuelezea alomofu.
(ii) Alomofu ni mofu mojawapo miongoni mwa mofu za mofimu moja kwani zina sura moja tu.. Popote zinapotokea hutokea na sura ileile na hazibadiliki.

Kwa mfano katika lugha ya Kiingereza kwa mfano, kiambishi tamati /s/ cha wingi kina maumbo mbadala yafuatayo:

  1. /s/ kama katika maneno cats, books
  2. /z/ kama katika maneno dogs, bags
  3. /iz/ kama katika maneno classes, boxes, flies
  4. / / kama katika neno sheep

Alomofu ni umbo jingine la mofu ileile moja kama
inavyojidhihirisha katika maneno motto, muuguzi na mwanafunzi. Tunaona kwamba, viambishi awali (m-), (mw-) na (mu-) vyote vinawakilisha mofimu moja ya ngeli ya kwanza. Katika lugha za Kibantu. Kwa hivyo, maumbo {m-}, {mu-}, na {mw-} ni alomofu zinazokilisha mofimu moja. Hivyo basi, alomofu ni maumbo mawili au zaidi yanayowakilisha mofimu moja. Alomofu hutokea katika mazingira maalum katika maneno. Mifano ufuatao unaonyesha alomofu katika lugha ya Kiswahili:

Mofimu ya umoja {mu}- {m}
{mu}
{mw}

Mifano ya Alomofu

(a) Mofu za wingi katika lugha ya Kiswahili
{wa-}- katika maneno wachawi, wanafiki, wanyonge
{mi-} – katika maneno miti, miembe, michoro n.k
{ma} – katika maneno matunda, mawele
{vi-} – katika maneno vikombe, vijiko, vichwa n.k

(b) Mifano ifutayo hudhurisha mofimu za njeo
Anacheza
Alicheza
Atachez

Katika mifano hiyo hapo juu, maumbo {-na-}, {-li-}, na {-ta-} nialomofu ambazo husetiri

Mofimu ya njeo.

(c)Vitenzi vifuatavyo hudhihirisha mofimu ya kutendea:
Kulia
Somea
Lilia
Lelea
Katika mifano hiyo hapo juu, maumbo {-i-}, {-e}, {-le} ni alomofu
ambazo husetiri mofimu ya kutendea.

Kwa machache hayo napenda kuwatikia kila la heri wapenzi wa somaji wa tovuti hii.

3 thoughts on “MOFOLOJIA YA KISWAHILI SANIFU

Leave a comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.